Mtangazaji na mdau waa burudani, Mwijaku, amemkosoa Mbunge wa Kigoma Mjini, Babalevo, kufuatia kitendo chake cha kuwalisha wananchi chakula cha bure siku ya Mwaka Mpya, akidai hatua hiyo haina mchango wa kudumu katika kubadilisha maisha ya watu wa Kigoma.
Akizungumza kwenye mahojiano na Rick Media, Mwijaku amesema Baba Levo amepata nafasi kubwa ya kuaminika na wananchi wa Kigoma, jambo linalompa wajibu wa kufanya maamuzi na miradi itakayobadilisha maisha yao kwa muda mrefu badala ya kutatua tatizo la siku moja.
Kwa mujibu wa Mwijaku, kutoa chakula cha bure ni jambo jema kwa wakati husika, lakini halitatui changamoto kubwa zinazowakabili vijana na wakazi wa Kigoma, hususan ukosefu wa ajira na fursa za maendeleo. Amesisitiza kuwa wananchi wanahitaji suluhisho endelevu litakalowawezesha kujitegemea.
Mwijaku ameongeza kuwa fedha zilizotumika kuwalisha wananchi zingeweza kuelekezwa katika miradi ya maendeleo, akitolea mfano kufunguliwa kwa Hub ya Vijana wa Kigoma ambayo ingewezesha vijana kubadilishana mawazo, kupata mafunzo, kushirikiana kwenye biashara na kufunguliwa kwa fursa mbalimbali za kiuchumi.