Sports news

Manchester United Yamfuta Kazi Ruben Amorim

Manchester United Yamfuta Kazi Ruben Amorim

Klabu ya Manchester United imetangaza rasmi kumfuta kazi Meneja Ruben Amorim kufuatia msururu wa matokeo yasiyoridhisha, ikiwa ni miezi 14 tu tangu achukue mikoba ya kuinoa timu hiyo.

Katika taarifa iliyotolewa na Manchester United, imeelezwa kuwa kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Darren Fletcher, ambaye alikuwa akihudumu kama Mkurugenzi wa Ufundi, ameteuliwa kushika nafasi ya kocha wa muda. Fletcher anatarajiwa kuiongoza United katika mchezo wao wa Ligi Kuu England dhidi ya Burnley siku ya Jumatano.

Uongozi wa klabu hiyo umefafanua kuwa, wakati Manchester United ikishika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi, uamuzi wa kumfuta Amorim umechukuliwa kwa moyo mzito ili kutoa nafasi ya mabadiliko yatakayoiwezesha timu kumaliza juu zaidi kwenye msimamo wa ligi.

Uamuzi huo pia unadaiwa kuchochewa na mvutano ulioibuka kati ya bodi ya klabu na Amorim kuhusu bajeti ya usajili, huku uhusiano wake na Mkurugenzi wa Michezo, Jason Wilcox, ukitajwa kudorora.

Kwa sasa, macho ya mashabiki na wachambuzi wa soka yameelekezwa kwa Darren Fletcher, wakisubiri kuona kama ataweza kuleta mabadiliko ya haraka na kuirejesha Manchester United kwenye njia ya ushindi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *