Mtangazaji na mdau wa burudani, Mwijaku, ameonyesha kusikitishwa na kitendo cha baadhi ya wasanii kumkataa kumsaidia meneja wa wasanii wa Bongofleva, Mkubwa Fela, wakati huu anapitia kipindi kigumu cha kuumwa.
Akizungumza kwa uchungu, Mwijaku amesema ameumia kumuona mtu aliyejitolea kwa muda mrefu kuwasaidia wasanii, anatengwa wakati huu anapitia matatizo ya kiafya. Ameongeza kuwa ameshangazwa na kitendo cha baadhi ya wasanii wakubwa kumkataa kumsaidia Mkubwa Fella licha ya kuwa na utajiri mkubwa.
Kwa mujibu wake, tukio hilo linapaswa kuwa funzo kwa jamii, akisisitiza kuwa si kila mtu anafaa kusaidiwa katika maisha. Ameeleza kuwa kuna watu ambao hubadilika mara wanapopata nafuu katika maisha.
Katika hatua nyingine, Mwijaku ametoa wito kwa mkongwe wa muziki wa Bongofleva Mwana FA kuingilia kati na kusaidia gharama za matibabu ya Mkubwa Fela, akisema mchango wa meneja huyo katika kulea vipaji na kukuza tasnia ya muziki hawezi kupuuzwa.