Rais William Ruto amemkaribisha rasmi streamer na YouTuber maarufu duniani, IShowSpeed, nchini Kenya huku akitaja Kenya kama taifa lenye hisia, msukumo na mvuto wa kipekee usiolinganishwa na nchi nyingine yoyote.
Kupitia video iliyochapishwa mtandaoni, Rais Ruto amesema Kenya siyo nchi ya kawaida bali ni mahali penye uhai na hisia zinazogusa mioyo ya watu. Ameeleza kuwa Kenya ni nyumbani kwa wote, taifa linalobeba roho ya ukarimu wa Kiafrika na uzuri wa kipekee unaoifanya ijulikane duniani kama chanzo cha maajabu na mshangao.
Kiongozi huyo, amebainisha kuwa ujio wa IShowSpeed ni fursa muhimu ya kuitangaza Kenya kimataifa, hasa kupitia majukwaa ya kidijitali yanayofuatiliwa na mamilioni ya vijana duniani. mesisitiza kuwa Kenya ina utajiri wa tamaduni, vipaji vya vijana, burudani na ubunifu wa kiteknolojia unaostahili kuonekana na kuthaminiwa kimataifa.
Kauli hiyo imepokelewa vyema na Wakenya wengi mitandaoni, wakieleza fahari yao kwa namna taifa linavyoendelea kujitangaza kama kituo cha burudani, utalii na ubunifu wa kisasa. Ziara ya IShowSpeed inaendelea kuzua gumzo, huku wengi wakisubiri kwa hamu kuona maudhui yatakayomulika maisha, utamaduni na vivutio vinavyoifanya Kenya kuwa taifa la kipekee.