Programu mpya ya simu ya mkononi iitwayo “Are You Dead?” imepata umaarufu mkubwa nchini China, hususan miongoni mwa vijana wanaoishi peke yao katika miji mikubwa. Programu hiyo humtaka mtumiaji kubonyeza kitufe kimoja kila siku kuthibitisha kuwa yuko hai na salama, ambapo taarifa hutumwa kwa mtu wa dharura aliyeteuliwa.
Kwa mujibu wa watengenezaji wake, endapo mtumiaji atashindwa kuthibitisha hali yake kwa siku mbili mfululizo, programu hutuma tahadhari kwa njia ya barua pepe kwa mtu wa dharura, ikionya kuwa huenda mtumiaji huyo yuko kwenye hatari au anahitaji msaada wa haraka.
Programu hiyo inalenga watu wanaoishi peke yao na ambao hawana ufuatiliaji wa karibu wa kila siku. Tofauti na programu nyingine za mawasiliano, haitaji simu, ujumbe wala mipangilio tata, bali inategemea uthibitisho rahisi wa kila siku.
Umaarufu wa programu hiyo unaakisi mabadiliko ya kijamii nchini China, ambapo idadi ya watu wanaoishi peke yao inaendelea kuongezeka, hasa katika miji mikubwa. Watumiaji wengi wamesema programu hiyo imewapa hisia ya usalama, huku wawekezaji wakionesha nia ya kuiunga mkono kama suluhisho linalochanganya teknolojia na ustawi wa kijamii.