Staa wa muziki wa Bongoflava, Harmonize, ametoa angalizo kwa wasanii wanaopanga kuachia nyimbo mpya wiki ijayo, akiwataka waahirishe mipango yao.
Kupitia mitandao ya kijamii, Harmonize ameweka wazi msimamo wake kwa maneno makali akisema wasanii watakaothubutu kuachia nyimbo zao juma lijalo huenda wakakosa kupata mapokezi mazuri sokoni.
Kwa mujibu wa Harmonize, muda huo ni maalum kwa ujio wa video mpya ya wimbo wake aliomshirikisha Mbosso ambayo anadai itatikisa tasnia ya muziki Afrika Mashariki.
Kauli ya Harmonize inakuja wakati ambapo wimbo wake uitwao Leo unaendelea kufanya vizuri sokoni, visualizer yake ikifikisha zaidi ya views milioni 5 kwenye mtandao wa YouTube. Lakini pia wimbo huo umeshika nafasi ya kwanza nchini Tanzania, jambo linaloonyesha nguvu na ushawishi mkubwa wa msanii huyo katika tasnia ya muziki.