Mrembo kutoka Kenya,Pritty Vishy, amejutia kuwa katika uhusiano wa kimapenzi na msanii Stevo Simple Boy, akisema kuwa kauli za hivi karibuni za msanii huyo zimemuumiza na kumshangaza kwa kiwango kikubwa.
Mrembo huyo wa mitandao ya kijamii amesema amesikitishwa na madai ya Stevo kwamba alitumia uhusiano wao kama njia ya kujipatia umaarufu. Kwa mujibu wa Pritty, kauli hizo hazina ukweli wowote, hasa ikizingatiwa kuwa wakati walipokuwa pamoja alikuwa mstari wa mbele kumkingia kifua Stevo katika vipindi vigumu.
Pritty ameeleza kuwa kipindi wanachumbiana alikuwa na umri wa miaka 21, huku Stevo akiwa na miaka 34, hali ambayo haikumzuia kusimama naye hata pale alipokuwa akikabiliwa na shutuma za kumnyanyasa licha ya tofauti yao ya umri.
Vishy, amefafanua kuwa hakuwahi kutumia jina la Stevo kwa manufaa binafsi, bali alimtetea kwa dhati pale alipokuwa akikabiliwa na lawama kutoka kwa umma.
Hata hivyo, Pritty amemtaka Stevo aachane naye kabisa na kuacha kuibua masuala ya uhusiano wao wa zamani, akisisitiza kuwa ni vyema aangazie familia yake na maisha yake ya sasa.