Msanii aliyeacha muziki wa kidunia na kugeukia Injili, Kush Tracy, amefunguka kuhusu maisha yake ya nyuma akieleza kuwa aliwahi kuishi kwenye uraibu wa pombe na matumizi ya mihadarati kwa kipindi kirefu kabla ya kubadili mwelekeo wa maisha na kuokoka.
Kupitia podcast ya Mwakideu Live, Kush Tracy amesema kulikuwa na kipindi ambacho aliweza kunywa pombe na kutumia mihadarati kwa wiki nzima bila kupumzika, hali aliyosema ilimharibu kimwili na kiakili.
Msanii huyo amesema wakati huo hakuwa na hofu wala malengo ya maisha, akifanya mambo bila kujali athari zake. Ametoa mfano wa jinsi uraibu huo ulivyomfanya kushiriki mapenzi kiholela akiwa mlevi kupindukia.
Msanii huyo ameongeza kuwa safari ya kuokoka haikuwa rahisi, lakini ilikuwa uamuzi muhimu uliobadili maisha yake kabisa.
Kush Tracy sasa anatumia ushuhuda wake kuwahimiza vijana kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na pombe kupita kiasi, akisisitiza kuwa mabadiliko yanawezekana kwa yeyote anayeamua.