Mwanamuziki mkongwe kutoka nchini Uganda, Jose Chameleone, anatarajiwa kuzindua kituo kipya cha redio jijini Bujumbura, Burundi, kitakachoitwa Chameleone FM.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vya karibu na msanii huyo, Chameleone amenunua kituo cha zamani cha Black FM, ambacho sasa kinatarajiwa kuanza upya chini ya jina jipya la Chameleone FM, hatua inayolenga kuimarisha uwepo wake katika sekta ya vyombo vya habari nchini Burundi.
Mbali na uwekezaji huo wa redio, ripoti zinaeleza kuwa Chameleone pia yupo katika hatua za mwisho za kufungua hospitali aliyoijenga katika eneo la Cankuzo. Inadaiwa kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi zake za kurudisha fadhila kwa wananchi wa Burundi kupitia huduma za kijamii, hususan katika sekta ya afya.
Hatua hizi za uwekezaji zinakuja baada ya ziara ya Chameleone nchini Burundi, ambapo mwishoni mwa mwaka jana alikutana na Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye. Katika kikao hicho, msanii huyo alieleza dhamira yake ya kuwekeza nchini humo na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.