Mwanamitandao Chief Godlove amefunguka sababu zilizopelekea kusitisha mpango wa kumsimamia kikazi aliyekuwa msanii wake, Pipi Jojo ambaye alimtambulisha kwenye tasnia ya muziki mwishoni mwa mwaka 2025.
Akizungumza na Bongo 5, Chief Godlove amesema taarifa zilizoibuliwa na Mwijaku zikidai kuwa alimpa ujauzito Pipi Jojo zilimletea madhara makubwa katika ndoa yake. Amesema madai hayo, ambayo anasisitiza hayakuwa ya kweli, yalizua mgogoro mkubwa nyumbani kwake na kusababisha sintofahamu iliyohitaji muda na jitihada kuimaliza.
Kwa mujibu wa Chief Godlove, kelele za mitandaoni na presha kutoka kwa jamii zilifanya iwe vigumu kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Pipi Jojo kama ilivyokuwa awali. Amesema kuwa uamuzi wa kutengana kikazi haukutokana na chuki au tofauti za kimkakati, bali ni kulinda familia yake na amani ya ndoa yake.
Hata hivyo, amewataka mashabiki kuendelea kumpa sapoti Pipi Jojo katika safari yake ya muziki, akisisitiza kuwa ana kipaji kikubwa na ana uwezo wa kufika mbali zaidi hata bila yeye kuwa meneja wake. Amesema anaamini msanii huyo ataendelea kung’ara na kufanikisha ndoto zake.