Teknolojia ya kutambua nyimbo ya Shazam sasa imeunganishwa rasmi ndani ya ChatGPT, hatua inayolenga kurahisisha zaidi namna watumiaji wanavyotambua na kufurahia muziki kupitia simu zao.
Kupitia kipengele hiki kipya, watumiaji wa ChatGPT wanaweza kusema “Shazam wimbo huu” au kuuliza “Huu ni wimbo gani?”, na mfumo utaanza kutumia microphone ya simu kusikiliza wimbo unaochezwa. Baada ya hapo, ChatGPT hushirikiana na huduma ya Shazam kutambua wimbo huo na kutoa taarifa zake, ikiwemo jina la wimbo na msanii.
Mbali na kutambua wimbo, watumiaji wanaweza pia kuomba ChatGPT iwaandalie playlist kulingana na nyimbo walizotambua au aina ya muziki wanaopenda. Playlist hiyo inaweza kuunganishwa moja kwa moja na majukwaa maarufu ya muziki kama Apple Music au Spotify.
Mabadiliko haya ni sehemu ya ushirikiano kati ya Apple na OpenAI, unaolenga kuboresha uzoefu wa watumiaji katika kugundua muziki na kusimamia maktaba zao za nyimbo kwa njia rahisi zaidi.
Kwa kuunganisha teknolojia ya utambuzi wa muziki ya Shazam na uwezo wa mazungumzo wa ChatGPT, watumiaji sasa wanatarajiwa kupata njia mpya na ya haraka ya kugundua na kusikiliza muziki wanaoupenda.