
Mwanamuziki chipukizi mwenye kipaji cha kipekee, Abigail Chams maarufu kama Abby Chams, ameweka historia mpya kwa kuonekana kwenye Jalada (Cover) ya toleo la Mei la jarida maarufu la Rolling Stone Africa. Katika toleo hilo, Abby ametajwa kama “Future of Music”, ikiwa ni ishara ya heshima kubwa kwa mchango wake unaokua kwa kasi katika tasnia ya muziki barani Afrika.
Kupitia ukurasa rasmi wa Instagram wa Rolling Stone Africa, waliandika:
“Abigail Chams aingia kwenye mwangaza – Kutoka kwenye ala za hisia hadi mashairi ya Kiswahili, Abigail Chams anawaalika wasikilizaji katika mazingira ya sauti ambapo mila inakutana na ubunifu.”
Jalada hilo linaonesha picha ya Abby akiwa na mtazamo wa kujiamini, akiwakilisha kizazi kipya cha wasanii wa Kiafrika wanaovuka mipaka kwa sauti, mitindo na ujumbe wao. Kutajwa kwake kama “Future of Music” ni uthibitisho wa upekee wa mtindo wake wa muziki unaochanganya ala za jadi, sauti za kisasa, na matumizi ya Kiswahili katika muziki wa kimataifa.
Abby Chams, ambaye ameendelea kung’ara kwa nyimbo zake zenye ujumbe wa kina na ladha ya kipekee ya Afro-soul, ameonekana kuendelea kuvunja vizingiti, hasa kwa wasanii wachanga wa kike kutoka Afrika Mashariki.
Mashabiki na wadau mbalimbali wa muziki wamempongeza Abby kwa hatua hiyo kubwa, wakisema kuwa huu ni mwanzo tu wa mafanikio makubwa zaidi.