
Mwanamuziki kutoka Kenya, Akothee, ameibuka na kutoa kauli yake kuhusiana na mgogoro unaoendelea kati yake na fundi seremala aliyemtengezea samani. Kupitia mitandao ya kijamii, Akothee ameeleza kwa kina kwamba fundi huyo hakutimiza masharti ya kazi kama walivyokubaliana.
Akothee amesema licha ya kutoridhishwa na kazi iliyofanyika, tayari alikuwa amemlipa fundi huyo asilimia 80 ya malipo yaliyokubaliwa. Alidai kuwa meza aliyoletwa haikukidhi viwango vya ubora aliokuwa ameelekeza, hivyo hakusita kuonyesha kutoridhishwa kwake.
“Sio kila mtu anayeitwa fundi anaelewa kazi. Nilimlipa 80% lakini alileta meza isiyokidhi viwango tulivyokubaliana,” aliandika Akothee.
Mwanamuziki huyo ambaye pia ni mfanyabiashara ameonya mafundi dhidi ya kutumia majina ya watu maarufu kujinufaisha kibiashara ilhali hawatimizi kazi kwa kiwango kinachotarajiwa. Aliongeza kuwa ana ushahidi wote wa mawasiliano na malipo aliyofanya.
“Naomba arudishe hela zangu na achukue meza yake. Sina haja nayo,” alisema kwa msisitizo.
Sakata hilo limevutia hisia mbalimbali mitandaoni, huku baadhi ya mashabiki wakimuunga mkono Akothee kwa kusimamia haki yake, huku wengine wakitaka pande zote mbili kusuluhisha suala hilo kwa njia ya amani.