Msanii asiyeishia na matukio kila leo, Akothee, ameonyesha kuchukizwa kwake na tabia ya baadhi ya wanaume wanaomfuata kupitia jumbe za faragha wakimtaka kimapenzi au hata kumuomba msaada wa kifedha.
Kupitia mitandao ya kijamii, Akothee amesema amechoshwa na wanaume anaowataja kuwa wazembe, ambao badala ya kufanya kazi na kujituma, wamegeuza mitandao ya kijamii kuwa sehemu ya kuomba mahusiano na misaada ya kifedha kutoka kwa wanawake waliopiga hatua kimaisha.
Akothee amewataka wanawake kupuuza kabisa wanaume wa sampuli hiyo, akisisitiza kuwa mwanamke hapaswi kubeba majukumu ya mwanaume mzima kwa misingi ya mapenzi.
Kauli yake inakuja siku chache baada ya kudai kuwa mwaka 2026 ataanza kuwaanika hadharani wanaume wanaomfuata kwa siri wakimuomba pesa, akisema tabia hiyo imevuka mipaka na haikubaliki katika ulimwengu wa sasa.