Msanii wa muziki wa hip hop nchini Kenya, Octopizzo, ameingia katika majonzi kufuatia kifo cha meneja wake na rafiki wa muda mrefu, Ongaya Vick, anayefahamika pia kwa jina la Cheeks Zone.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Octopizzo ameeleza huzuni yake kuu akitangaza msiba huo, akisema Ongaya hakuwa tu meneja bali pia alikuwa mtu aliyemwamini na kumtia moyo tangu mwanzo wa safari yake ya muziki.
Kwa mujibu wa Octopizzo, Ongaya ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuona uwezo wake wakati wengi walikuwa na mashaka kama muziki wa rap ungeweza kumtoa kisanaa. Amesema tangu mwaka 2009, Ongaya amekuwa nguzo kuu ya ubunifu nyuma ya chapa ya Octopizzo, akisaidia kuijenga hadi kufikia mafanikio ya kimataifa.
Rapa huyo ameeleza kuwa imani na maono ya marehemu yalimsaidia si tu katika taaluma yake ya muziki, bali pia kumfanya kuwa mtu bora zaidi maishani.
Kwa sasa, marafiki na jamaa wanakusanyika katika makazi ya familia ya Ongaya eneo la Woodley, Nairobi, kwa maandalizi ya mazishi. Marehemu anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake Kakamega, ambako familia itamkumbuka kama mtu mwenye moyo wa upendo, ubunifu, na uongozi.