
Kampuni ya Apple imeanza kutengeneza mfumo mpya wa uendeshaji (operating system) ambao unalenga kubadilisha kabisa jinsi vifaa vya nyumbani vinavyofanya kazi. Taarifa zinaeleza kuwa mfumo huo mpya utafanya kazi katika aina mbalimbali za vifaa vya nyumbani kama spika zenye skrini ndogo, roboti wa usafi (cleaning robots), vifaa vya kielektroniki vya nyumbani, na vifaa vya kiusalama kama vile kufuli za milango.
Mfumo huo unatajwa kuwa na muundo unaofanana na tvOS na watchOS, mifumo ambayo tayari inatumika katika Apple TV na saa janja za Apple. Lengo kuu ni kufanya vifaa vya Apple viweze kuzungumza kwa urahisi kupitia jukwaa moja la kipekee, lenye uwezo wa kutumia akili bandia (AI) na huduma za kisasa kama Siri na FaceID.
Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, mfumo huu mpya utawezesha vifaa kutumia FaceID kwa kufuli za milango, huku Siri ikibaki kuwa kiini cha mawasiliano kati ya mtumiaji na kifaa. Aidha, mfumo huu utakuja na programu muhimu kama Kalenda, Kamera, Muziki, Notes pamoja na Siri kama msaidizi wa kidijitali.
Apple inatarajia kuzindua rasmi mfumo huu mwishoni mwa mwaka huu au mapema mwaka 2026, hatua ambayo inatazamiwa kuleta mapinduzi makubwa katika teknolojia ya nyumbani na kuweka Apple katika nafasi nzuri ya kushindana katika soko la smart home devices.
Mashabiki wa teknolojia na watumiaji wa vifaa vya Apple wanasubiri kwa hamu kuona mapinduzi haya mapya yatakavyoleta urahisi, usalama na ufanisi zaidi katika maisha ya kila siku ya nyumbani.