Kampuni ya teknolojia Apple imetangaza kuwa kuanzia mwezi Machi mwaka huu itaongeza idadi ya matangazo katika sehemu ya utafutaji, yaani Search, kwenye App Store.
Kwa mujibu wa taarifa ya Apple, mabadiliko hayo yataanza mwezi wa tatu na yataathiri watumiaji wa iPhone, Mac, pamoja na vifaa vingine vya Apple. Watumiaji wanatarajiwa kuona matangazo mengi zaidi wanapotafuta programu ndani ya App Store.
Apple imesisitiza kuwa licha ya ongezeko la matangazo, itahakikisha masuala ya faragha na usalama wa watumiaji yanaendelea kupewa kipaumbele.
Hapo awali, matangazo yalikuwa yakionekana juu tu ya matokeo ya utafutaji. Hata hivyo, kuanzia Machi, matangazo yataonekana pia katika sehemu za chini za matokeo, na idadi yake itaongezeka.
Wachambuzi wa masuala ya teknolojia wanasema hatua hiyo inaonesha mwelekeo wa Apple kufuata mfano wa Google, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitegemea matangazo kama chanzo kikuu cha mapato.