Entertainment

Azawi Kutumia Muziki Kupaza Sauti za Waganda Walionyimwa Haki

Azawi Kutumia Muziki Kupaza Sauti za Waganda Walionyimwa Haki

Mwanamuziki wa Uganda, Priscilla Zawedde maarufu kama Azawi, ameweka wazi dhamira yake ya kutumia muziki kama chombo cha kupaza sauti dhidi ya dhuluma na ukosefu wa haki nchini mwake. Hii ni baada ya takriban miaka miwili ya kuikosoa serikali hadharani kupitia majukwaa mbalimbali.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini Uganda, Azawi alieleza kuwa yupo mbioni kuingia studio kurekodi nyimbo za mapinduzi zenye ujumbe mzito unaoelezea machungu na hali halisi ya wananchi wa kawaida.

“Nataka kuonesha maumivu ya Waganda wengi kupitia muziki wangu,” alisema Azawi. “Nafanya kazi juu ya hilo, na label yangu Swangz Avenue wanaheshimu maoni na mtazamo wangu.”

Akiwa chini ya usimamizi wa lebo ya Swangz Avenue, Hitmaker huyo wa ngoma ya “Talking Stage” alisisitiza kuwa hana hofu ya kupoteza nafasi yake kwenye lebo hiyo, endapo msimamo wake wa kisanii hautaungwa mkono.

“Ikiwa hawatataka kufanya kazi nami kwa sababu ya nyimbo hizo, ni sawa tu. Nitajiondoa,” alisema kwa msimamo thabiti.

Azawi anaelekea kufungua ukurasa mpya wa muziki wenye uzito wa kijamii na kisiasa, hatua ambayo huenda ikamuweka kwenye mgongano na serikali au hata wasimamizi wake wa kazi za usanii lakini pia inaweza kumweka katika nafasi ya kipekee kama msanii anayesimama kwa ajili ya watu wake.

Hata hivyo mashabiki wake wameonyesha msisimko mkubwa mtandaoni, wakimpongeza kwa ujasiri na nia ya kutumia muziki kama silaha ya kupigania haki na kuunganisha jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *