Msanii na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Babalevo, ameahidi kuendeleza utamaduni wa kukutana na kula pilau pamoja na wananchi wa jimbo lake katika kila sikukuu, akisema kuwa ni njia muhimu ya kuimarisha mshikamano, umoja na ukaribu kati ya viongozi na wananchi.
Akiongea wakati sikukuu ya kukaribisha mwaka mpya wa 2026, Babalevo amesema kuwa tukio alilolianda la Pilau Day limeonyesha wazi namna matukio ya kijamii yanavyoweza kuwakutanisha watu wa makundi mbalimbali na kujenga mahusiano ya karibu ndani ya jamii.
Mbunge huyo ameongeza kuwa ataendelea kuweka mipango itakayohakikisha wananchi wanakutana, kushirikiana na kufurahia pamoja katika mazingira ya amani na upendo licha ya ukosoaji kutoka kwa wapinzani wake.
Babalevo ametoa kauli hiyo baada ya kushuhudia furaha na mshikamano mkubwa wa wananchi wa Kigoma Mjini waliojumuika kwa pamoja kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya, ambapo wananchi walikula pilau kwa pamoja na kupata burudani kutoka kwa wasanii wa Bongo Fleva waliopanda jukwaani na kuwapagawisha mashabiki kwa nyimbo zao zilizopendwa.