
Msanii mashuhuri wa muziki nchini Kenya, Kevin Bahati, maarufu kama Bahati, amefichua kuwa hakuwahi kunyoa nywele zake aina ya rasta kama ilivyodhaniwa awali.
Kupitia chapisho katika ukurasa wake rasmi wa Instagram, Bahati alieleza kuwa picha zilizokuwa zikimuonesha akiwa hana nywele zilihaririwa kwa makusudi, kama sehemu ya mkakati wa kisanaa.
Katika ujumbe wake, Bahati aliandika:
“Nimechoka kujificha pia editor anasema amechokaaaa kunibadilisha vichwa.”
Kauli hiyo imekuwa gumzo mitandaoni, ikiwa ni mara ya kwanza kwa msanii huyo kufichua ukweli kuhusu mabadiliko hayo ya muonekano yaliyozua mijadala miongoni mwa mashabiki na wafuasi wake.
Bahati alifafanua kuwa hatua ya kuhariri picha hizo ilikuwa sehemu ya mbinu ya ubunifu ili kuvutia hisia na kuanzisha mwelekeo mpya katika kazi zake za muziki. Amedokeza kuwa hakuwahi kuwa na nia ya kuwadanganya mashabiki wake, bali alitumia mbinu hiyo kama njia ya kuwasilisha maudhui kwa mtazamo tofauti.
“Ilikuwa ni njia ya kuwasiliana kisanii. Sikunyowa rasta, ila nilitaka kuanzisha sura mpya ya ubunifu,” alisema kupitia mitandao ya kijamii.
Taarifa hiyo imepokelewa kwa hisia mseto. Wakati baadhi ya mashabiki wameonyesha kuelewa na kupongeza ubunifu wa Bahati, wengine wameeleza kusikitishwa na kile walichokiona kuwa ni udanganyifu wa makusudi. Hata hivyo, mjadala huu unaashiria athari kubwa aliyo nayo Bahati katika tasnia ya burudani nchini.
Kwa mara nyingine, Bahati ameweza kuvuta hisia za umma kupitia mitandao ya kijamii, akitumia mbinu isiyo ya kawaida kufikisha ujumbe wake. Anaendelea kudhihirisha kuwa katika ulimwengu wa kisasa wa burudani, ubunifu hauishii kwenye muziki pekee, bali pia katika namna ya kujieleza na kuwasiliana na mashabiki.