Entertainment

Bahati Alalamikia Chuki na Wivu Kutoka kwa Wasanii wa Nyimbo za Injili

Bahati Alalamikia Chuki na Wivu Kutoka kwa Wasanii wa Nyimbo za Injili

Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Bahati, ameshindwa kuvumilia ukosoaji anaoupata mtandaoni baada ya kuonekana akilia hadharani akielezea machungu anayopitia kutokana na chuki na wivu kutoka kwa baadhi ya wasanii wenzake, hasa wale wa muziki wa Injili.

Kupitia video aliyoshiriki kwenye mitandao ya kijamii, Bahati ameonekana mwenye majonzi akisema kwamba kama Mungu angekuwa binadamu, huenda maisha yake yasingekuwa salama kutokana na chuki na husuda za watu. Ameeleza kuwa mara nyingi amekuwa akihukumiwa kwa maamuzi yake ya kisanii na maisha yake binafsi, huku wengi wakisahau kwamba yeye ni binadamu wa kawaida anayekosea kama wengine.

Bahati ambaye amepata ukosoaji mkubwa kutoka kwa mashabiki, ameongeza kuwa kila anapojaribu kuinuka, baadhi ya watu wamekuwa wakitamani ashindwe, jambo ambalo limekuwa likimuumiza zaidi akiona baadhi ya wasanii wa Injili wakiendelea kumuombea mabaya badala ya kumtakia heri.

Hata hivyo ameahidi kuachia wimbo wake mpya wa kumshukuru Mungu kwa mafanikio aliyoyapata, akisema ni ushuhuda wa jinsi Mungu amemuinua licha ya changamoto na maneno ya watu.

Bahati ameeleza kuwa hajawahi kujiona mkamilifu, lakini anaamini baraka zake zinatoka kwa Mungu. Amesema watu wengi hawajui machozi na maumivu aliyopitia ili kufika alipo sasa, na ndiyo sababu ameamua kutumia muziki wake mpya kama sala ya shukrani.

Kauli ya Bahati inakuja muda mfupi baada ya kuomba mashabiki zake msamaha kutokana na miendo yake inayokwenda kinyume na maadili ya jamii kwa kujihusisha na maudhui yanayohamasisha ngono.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *