
Staa wa muziki, Bahati, amejipata kwenye lawama baada ya kushindwa kutimiza ahadi yake ya kutoa shilingi milioni moja kwa wachezaji wa Harambee Stars kufuatia ushindi wao dhidi ya Morocco kwenye michuano ya CHAN 2024.
Katika mahojiano, baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa wamefichua kuwa fedha walizopokea zilikuwa zawadi kutoka kwa Rais William Ruto, na siyo kutoka kwa Bahati kama ilivyokuwa imetangazwa awali.
Wiki iliyopita, msanii mwenzake Willy Paul alimkosoa vikali Bahati akimtaka atimize ahadi yake kwa timu hiyo, hatua iliyomlazimu Bahati kujitokeza na kujitetea. Alidai kuwa hakuweza kukamilisha ahadi hiyo kwa sababu sheria za Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) zilimzuia kufika kambini kuonana moja kwa moja na wachezaji.
Hata hivyo, mashabiki na wadau wa soka wameendelea kumtupia lawama wakimtaka awe na uwazi na uadilifu katika kutoa ahadi zake, hasa pale zinapohusiana na masuala ya taifa.