
Bifu kati ya msanii mkongwe Jose Chameleone na msanii mtukutu Alien Skin limechukua mwelekeo mpya baada ya mmoja wa walinzi wa Alien Skin, aitwaye Punisher Pro Max, kudaiwa kushushiwa kichapo cha mbwa na wanachama wa Leone Island usiku wa Alhamisi.
Taarifa zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea kufuatia mfululizo wa vitisho na matusi kati ya kambi ya Chameleone na ile ya Fangone Forest inayoongozwa na Alien Skin. Baunsa huyo anadaiwa kuwa katika mstari wa mbele kumtetea bosi wake, hali iliyochochea uhasama na kusababisha mashambulizi hayo.
Video zilizozagaa mitandaoni zilimuonyesha Chameleone akionya vikali kambi ya Alien Skin, akisisitiza kuwa atawafundisha nidhamu kwa nguvu ikiwa wataendelea kumvunjia heshima.
Kwa upande wake, Alien Skin alijibu vitisho hivyo kwa msimamo mkali, akisisitiza kuwa haogopi mapambano na yupo tayari kukabiliana na Chameleone pamoja na ndugu zake Pallaso na Weasel Manizo.
Kichapo cha baunsa huyo kimeibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki, baadhi wakionya kuwa bifu hili linaweza kuathiri taswira ya muziki wa Uganda na hata kupelekea vurugu zaidi endapo pande zote mbili hazitatuliza hasira.