Entertainment

Bebe Cool Afichua Lengo la Ziara Yake ya Siku 7 Nchini Kenya

Bebe Cool Afichua Lengo la Ziara Yake ya Siku 7 Nchini Kenya

Mwanamuziki nguli kutoka Uganda, Bebe Cool, amefichua kuwa ziara yake ya siku saba nchini Kenya inalenga zaidi kushirikiana na wasanii wa humu nchini na kujenga mahusiano mapya katika tasnia ya muziki wa Afrika Mashariki.

Akizungumza wakati wa mahojiano  jijini Nairobi, Bebe Cool alieleza kuwa anatamani kufanya kazi na wasanii wakubwa wa Kenya akiwemo Bien wa Sauti Sol, pamoja na wanamuziki waliotamba kwa miaka mingi kama Wyre na Nazizi.

“Kenya ni nyumbani kwangu. Muziki wetu wa Afrika Mashariki unaweza kuimarika zaidi tukishirikiana. Niko hapa kwa wiki moja lakini nina malengo ya muda mrefu, si tu collabo moja,” alisema Bebe Cool kwa msisitizo.

Mbali na wasanii, Bebe Cool pia alionyesha nia ya kufahamiana na DJs wapya wa Kenya, akisema wao ni kiungo muhimu katika kusukuma muziki wa kanda hii kimataifa.

Mashabiki wa muziki wa Afrika Mashariki wamepokea taarifa hiyo kwa furaha, wengi wakitarajia mashirikiano ya kuvutia ambayo yatabeba ladha ya muziki wa Kenya na Uganda. Wadau wa burudani wanasema hatua hiyo inaweza kufungua milango ya ushawishi wa kimataifa kwa wasanii wa eneo hili.