Mwimbaji nyota wa Injili nchini Kenya, Betty Bayo, amezikwa leo nyumbani kwake, Mugumo Estate katika kaunti ya Kiambu.
Maelfu ya waombolezaji, wakiwemo viongozi wa kidini, wasanii wenzake, na mashabiki waaminifu, walijitokeza kwa wingi kushiriki ibada ya mazishi iliyofanyika katika uga wa Ndumberi kutoa heshima zao za mwisho.
Waliohudhuria mazishi hayo wakiwemo viongozi wa kisiasa walimtaja marehemu Betty Bayo kama mtu aliyekuwa na mchango mkubwa na chanya kwa taifa kupitia muziki wake. Wasanii wenzake walisema kwamba Bayo alikuwa mfano wa kuigwa na alileta mapinduzi katika sekta ya muziki wa Injili.
Betty Bayo atakumbukwa kwa nyimbo zake zilizojenga na kutoa matumaini kwa Wakenya wengi, na kifo chake kimeacha pengo kubwa katika tasnia ya sanaa na injili nchini Kenya.
Mwanamuziki huyo alifariki mapema mwezi huu baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa damu aina ya leukemia, ambao alikuwa akipambana nao kwa muda kabla ya kifo chake.