
Msanii aliyegeukia siasa, Bobi Wine, ameendelea kutoa maoni yake kuhusu changamoto zinazokumba sekta ya muziki nchini Uganda. Wine, ambaye alijipatia umaarufu mkubwa katika muziki kwa zaidi ya miaka kumi na tano kabla ya kuingia kwenye siasa na hata kuwania urais, anasema sekta hiyo sasa inadhibitiwa na makundi yenye ushawishi makubwa yanayofanya kazi kwa niaba ya serikali.
Kwa mujibu wake, serikali inalenga kuhakikisha hakuna msanii mwingine anayeweza kufikia kiwango cha ushawishi alichopata kupitia muziki wake, hivyo kuzuia sanaa kutumika kama chombo cha kuibua sauti za upinzani. Anaeleza kuwa muziki nchini humo umekuwa chombo kinachodhibitiwa kwa karibu, ambapo kila kinachozalishwa studio kinasimamiwa kwa lengo la kudhibiti ujumbe unaofika kwa wananchi.
Licha ya kuingia kwenye siasa, Bobi Wine ameendelea kurekodi na kutoa nyimbo, akisisitiza kuwa wasanii wana jukumu la kueleza hali halisi ya jamii. Anawahimiza wanamuziki wenzake kutumia sanaa si tu kwa burudani, bali pia kama jukwaa la kuzungumzia changamoto za kijamii na dhuluma zinazowakumba wananchi.
Kauli hizi zinajiri wakati sekta ya muziki nchini Uganda inaendelea kupanuka kibiashara, lakini changamoto za udhibiti wa kisiasa na mashindano ya kifedha kati ya wasanii na serikali zikibaki kuwa kikwazo kikubwa kwa ukuaji wake.