
Mwanamuziki nyota wa Marekani, Britney Spears, hatimaye amezungumzia tukio lililoripotiwa kuhusu madai ya kukaidi maagizo ya kuacha kuvuta sigara akiwa ndani ya ndege. Kupitia chapisho aliloweka kwenye ukurasa wake wa Instagram, Spears ameelezea hali halisi ya kilichotokea, huku akikanusha kwa ucheshi madai ya kusababisha usumbufu, ambayo yamesambaa sana kwenye mitandao ya kijamii.
Katika maelezo yake, Spears amesimulia kwa mtindo wa mzaha kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza kunywa pombe aina ya vodka, jambo ambalo lilimfanya ahisi msisimko wa kipekee. Ameongeza kuwa alishangazwa na namna viti vya ndege hiyo vilivyokuwa na sehemu za kuweka vinywaji upande wa nje, tofauti na ilivyozoeleka.
“Me yesterday!!! It’s actually incredibly funny!!! Some planes I’ve been on you can’t smoke mostly but this one was different because the drink holders were on outside of seat!!! Confession it was my first time drinking VODKA!!! I swear I felt so SMART.” Aliandika.
Kauli hiyo imekuja baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa Spears alipuuza maelekezo ya wahudumu wa ndege waliomtaka azime sigara. Hata hivyo, kwa mtindo wake wa kipekee, alichagua kutoa ufafanuzi kwa njia ya ucheshi na simulizi ya kibinafsi.
Chapisho hilo limezua hisia tofauti miongoni mwa mashabiki wake. Wapo waliomtetea kwa kusema kuwa kila mtu hukosea mara moja moja, huku wengine wakieleza wasiwasi wao kuhusu tabia hiyo, hasa kwa mtu mwenye ushawishi mkubwa kama yeye.
Hadi sasa, haijafahamika ikiwa tukio hilo litachukuliwa kama ukiukwaji wa sheria za usalama wa anga, lakini Spears anaonekana kulichukulia kwa wepesi na bashasha kama ilivyo kawaida yake.