
Penzi la Vera Sidika linaonekana kuendelea kumtesa msanii wa muziki Brown Mauzo, hii ni baada ya kukiri hadharani kwamba bado anampenda sosholaiti huyo licha ya kutengana kwao miezi kadhaa iliyopita.
Mauzo amefunguka kupitia majibu kwa shabiki mmoja aliyemwandikia mtandaoni akisema walipendeza sana akiwa na Vera. Katika jibu lake, msanii huyo alikubali kuwa bado moyo wake haujamtoa Vera na kwamba anatamani kama wangeweza kurudiana.
Kwa mujibu wa Mauzo, uhusiano wake na Vera haukuwa wa kawaida kwani ulimjengea familia na kumpa mtoto, jambo analolitaja kama kumbukumbu na baraka kubwa katika maisha yake. Ameeleza kwamba Vera ataendelea kubaki mtu wa kipekee moyoni mwake kwa sababu ya nafasi aliyopewa katika maisha yake.
Uhusiano wa wawili hao uliwahi kuwa gumzo kubwa mitandaoni, uliojaa matukio ya kifahari, safari za kifamilia na hadithi za kimapenzi zilizoshirikishwa kwa mashabiki. Hata hivyo, baadaye walitangaza kuachana, kila mmoja akichukua mwelekeo tofauti. Vera alirudi kujikita katika biashara na maisha ya mitindo, huku Mauzo akijitahidi kurejea kwa nguvu kwenye muziki.
Kauli yake ya sasa imeibua hisia mseto mitandaoni, baadhi ya mashabiki wakimtia moyo kutafuta njia ya kusuluhisha tofauti zao na kumrudisha Vera, huku wengine wakimtaka akubaliane na hali na kuendelea mbele bila kumshikilia penzi la zamani.