
Msanii wa muziki kutoka Uganda, Bruno K, amekanusha vikali tuhuma za kusababisha kifo cha mwimbaji wa Injili kutoka Rwanda, Gogo Gloriose, aliyefariki dunia nchini Uganda tarehe 4 Septemba baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Bruno K amesema kuwa aliumizwa sana na madai ya baadhi ya wanablogu wa Uganda ambao walieneza uvumi kuwa alimfanyisha kazi kupita kiasi Gogo, jambo ambalo lilidaiwa kuchangia kifo chake, ili kumchafua mbele ya mashabiki wa Rwanda.
Akipiga stori na Royal FM, amesema hatua ya kubebeshwa lawama kwa misingi ya uongo ni ya kikatili, akisisitiza kwamba lengo lake lilikuwa kumuinua Gogo kisanii na kumsaidia kupiga hatua katika muziki.
Bruno K pia ameonyesha masikitiko yake kwa namna baadhi ya watu walivyopuuza kipaji cha marehemu wakati akiwa hai, lakini baada ya kifo chake wakaanza kuonyesha mapenzi makubwa kwake.
Hata hivyo ametoa wito kwa mashabiki kuacha kupotoshwa na simulizi za uongo, badala yake waonyeshe mshikamano na familia ya Gogo katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.