
Msanii wa muziki wa hip-hop nchini Marekani, Cardi B, amewashangaza mashabiki na wachambuzi wa muziki baada ya kuonekana akizunguka mtaani ya New York akitangaza kwa mikono yake mwenyewe albamu yake mpya “Am I The Drama.”
Tukio hilo lililoshuhudiwa na wapita njia na mashabiki wake limeibua mitazamo tofauti. Wapo wanaoona hatua hiyo kama mkakati wa kibunifu wa kumfanya msanii huyo aendelee kuwa karibu na mashabiki wake na kuonesha unyenyekevu katika tasnia ambayo mara nyingi hutegemea matangazo makubwa ya kibiashara. Hata hivyo, upande wa pili wa maoni unasema ni dalili za kukata tamaa na ishara kwamba mradi huo huenda unakumbwa na changamoto za kupenya sokoni kabla hata ya kutoka rasmi.
Kwenye mitandao ya kijamii, mjadala umechacha. Wafuasi wake wanamsifu kwa ujasiri wa kwenda mitaani na kujibebea jukumu la kutangaza kazi yake badala ya kutegemea matangazo ya kibiashara pekee. Lakini wakosoaji wanadai hatua hiyo inadhihirisha presha anayokabiliana nayo, hasa katika soko la muziki lenye ushindani mkali ambapo wasanii wapya na wakongwe huachia miradi kila mara.