
Staa wa muziki wa Hip Hop Cardi B anakabiliwa na kesi ya kisheria kufuatia tukio la mwaka 2023 ambapo alinaswa kwenye video akimrushia shabiki wake kipaza sauti wakati wa onyesho moja jijini Las Vegas, Marekani.
Kwa mujibu wa hati za mahakama zilizowasilishwa hivi karibuni, shabiki huyo ambaye jina lake halijawekwa wazi, anadai kuwa aliumia baada ya Cardi B kurusha kipaza sauti kwa hasira, kitendo kinachodaiwa kuwa ni shambulio, unyanyasaji wa mwili na uzembe.
Tukio hilo lilitokea wakati wa onyesho la Cardi B mwezi Julai 2023, ambapo inasemekana msanii huyo alikasirishwa na kitendo cha shabiki kumrusha kinywaji akiwa jukwaani. Katika kile kinachoelezwa kuwa ni kisasi, Cardi alionekana akirusha kipaza sauti kwa nguvu kuelekea kwenye kundi la mashabiki.
Ingawa hakukuwa na mashtaka ya jinai yaliyowasilishwa wakati huo, kesi hii mpya inaweza kumgharimu Cardi B fedha nyingi na kuathiri jina lake kwenye muziki. Wakili wa mlalamikaji anasema mteja wake alipata majeraha ya mwilini na pia mshtuko kutokana na tukio hilo.