Mwanamitandao kutoka Tanzania, Chief Godlove, amesema kuwa wivu, ujuaji mwingi, ubishi na kutotamani kuona wengine wakifanikiwa ni miongoni mwa sababu kuu zinazowakwaza vijana wengi wa Tanzania kushindwa kujijenga kiuchumi na kufikia ndoto za kuwa matajiri.
Kupitia mitandao yake ya kijamii, Chief Godlove amehoji kwa nini vijana wa Tanzania wenye umri wa miaka 35 kushuka chini wanaendelea kukumbwa na changamoto za kifedha, ilhali vijana wa nchi jirani kama Kenya, Uganda na Zambia wanaonekana kuanza mapema kujenga mali na kuwa na mitaji mikubwa ya kibiashara.
Kwa mujibu wa Chief Godlove, tatizo kubwa si ukosefu wa fursa bali ni mtazamo na tabia miongoni mwa vijana wenyewe. Amesema wengi hupoteza muda mwingi katika ubishi, kujiona wanajua kila kitu na kuwakatisha tamaa wenzao badala ya kushirikiana, kujifunza na kusaidiana kufikia mafanikio.
Mwanamitandao huyo, ameongeza kuwa baadhi ya vijana hawapendi kuona watu wanaowafahamu wakifanikiwa, hali inayochangia chuki, maneno hasi na kuvunjiana moyo badala ya kuhamasishana kufanya kazi kwa bidii na nidhamu.