Entertainment

Chris Brown Akamatwa Jijini Manchester kwa Tukio la Mwaka 2023

Chris Brown Akamatwa Jijini Manchester kwa Tukio la Mwaka 2023

Msanii nyota wa muziki wa R&B kutoka Marekani, Chris Brown, ameripotiwa kukamatwa jijini Manchester, Uingereza, muda mfupi baada ya kutua nchini humo kwa ndege binafsi (private jet).

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya usalama, maafisa wa Metropolitan Police (Met) walimkamata msanii huyo mara baada ya kubaini uwepo wake jijini humo. Kukamatwa kwake kunahusishwa na tukio la mwaka 2023, ambapo alidaiwa kumpiga kwa chupa ya mvinyo mtayarishaji wa muziki wa London aitwaye Abe Diaw, kitendo kilichosababisha majeraha makubwa hadi kusababisha kupoteza fahamu kwa muda.

Chris Brown kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano ya kina, huku uchunguzi ukiendelea kubaini mazingira kamili ya tukio hilo.

Baada ya tukio hilo la mwaka jana, Abe Diaw alimfungulia Chris Brown kesi ya madai, akitaka alipwe fidia ya takribani dola milioni 16 za Marekani (zaidi ya shilingi bilioni 2.1 za Kenya), kwa madai ya majeraha ya kudumu, usumbufu wa kisaikolojia na kupoteza mapato kutokana na kushindwa kuendelea na kazi ya muziki kwa muda.

Mpaka sasa, Chris Brown bado hajatoa taarifa rasmi kupitia timu yake ya mawakili wala mitandao yake ya kijamii kuhusu kukamatwa kwake.

Hii si mara ya kwanza kwa Chris Brown kukumbwa na matatizo ya kisheria. Licha ya mafanikio makubwa katika muziki, amewahi kujikuta matatani mara kadhaa kutokana na matukio ya fujo au unyanyasaji. Tukio hili jipya linaongeza orodha ndefu ya changamoto za kisheria zinazomwandama nyota huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *