
Rais wa Chama cha Wanamuziki Uganda (UMA), Cindy Sanyu, ametangaza mpango wa kuwasilisha rasmi malalamiko kwa Rais Yoweri Museveni kuhusu changamoto zinazowakumba wanamuziki wanaoamua pia kujihusisha na siasa za upinzani.
Cindy amesema kuwa serikali mara nyingi imekuwa ikidhoofisha taaluma ya wasanii wanaoingia katika ulingo wa kisiasa, jambo analoliona kama kikwazo kwa maendeleo ya tasnia ya muziki nchini humo.
Kwa mujibu wa mwanamuziki huyo, suala hilo atalibua katika kikao kijacho ambacho viongozi wa UMA wanatarajia kufanya na Rais Museveni. Amesisitiza kuwa hoja yake kuu itakuwa ni kutaka kuwepo na utofauti kati ya taaluma ya muziki na ile ya kisiasa, ili wanamuziki waweze kufanikisha malengo yao bila kudhalilishwa kwa misimamo yao ya kisiasa.
Cindy, ambaye ni mmoja wa wanamuziki wakongwe na mashuhuri nchini Uganda, amesema nia yake ni kuhakikisha kuwa muziki hauchukuliwi kama kikwazo kwa yeyote anayeamua kujaribu siasa, bali kila taaluma ipewe heshima yake bila kuathiri nyingine.