
Msanii maarufu wa hip hop, DaBaby, amepata ushindi wa kisheria baada ya jaji mmoja wa Los Angeles kutupilia mbali madai ya kushambulia yaliyowasilishwa na Brandon Bills, ndugu wa aliyekuwa mpenzi wake, DaniLeigh, kuhusu ugomvi uliotokea kwenye uwanja wa bowling mwaka 2022.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Billboard Hip Hop, jaji alitupilia mbali kesi hiyo kwa sababu ya kushindwa kumkabidhi DaBaby hati za madai ndani ya muda uliowekwa kisheria.
Licha ya ushindi huo, DaBaby bado anakabiliwa na madai ya kifedha yanayotokana na uharibifu wa mali katika uwanja huo wa bowling, ambapo waendeshaji wa sehemu hiyo wanadai fidia kupitia dai la kisheria la “indemnity” (fidia kwa uharibifu uliofanywa na mteja wake). Kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa rasmi mnamo msimu wa vuli wa mwaka 2026.
Ugomvi huo wa hadharani ulichukua nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari mwaka 2022, baada ya video za DaBaby na Brandon Bills wakizozana na kupigana hadharani kusambaa mitandaoni. Tukio hilo lilizua hisia kali kutoka kwa mashabiki na wanaharakati wa haki za kijamii.
Kwa sasa, ingawa amejinasua kwenye madai ya moja kwa moja ya kushambulia, DaBaby anasalia na safari ya kisheria mbele yake kuhusu athari za tukio hilo kwa biashara ya uwanja wa bowling.