
Msanii wa muziki nchini Kenya, Daddy Owen, ameendelea kutoa ushuhuda wa ndani kuhusu maisha yake, amefunguka kwamba mojawapo ya majuto makubwa maishani mwake ni kutokuanzisha familia mapema akiwa kijana.
Kwenye mahojiano na podcast ya Mwakideu Live, Daddy Owen amesema anatamani angeanza familia mapema alipokuwa katika miaka yake ya 20. Ameeleza kuwa wakati huo alikuwa amejijengea misingi imara ya kifedha, ikiwemo kumiliki nyumba kubwa ya vyumba vitano, lakini badala ya kusikiliza ushauri wa baba yake, alijikita zaidi kwenye starehe na kujivinjari na marafiki.
Kwa mujibu wa msanii huyo, ingawa sasa ana watoto wawili aliowapata mwishoni mwa miaka yake ya 30, anatamani angeweka kipaumbele kwa ndoa na familia mapema. Hitmaker huyo wa Mbona, amesema kuchelewa kwake kumefanya atafakari sana kuhusu nafasi na baraka ambazo familia huleta mapema maishani.
Kauli yake imeibua maoni tofauti miongoni mwa mashabiki. Baadhi wamesema ushuhuda wake ni funzo kwa vijana kuangalia mbali na kuepuka kupoteza muda kwenye starehe, huku wengine wakimtia moyo kwamba bado ana nafasi ya kujenga maisha yenye furaha pamoja na familia yake.