Mke wa Mkubwa Fella, ameibuka na madai mazito dhidi ya Diamond Platnumz akisema kuwa kwa sasa staa huyo wa muziki amewazimia kabisa simu liicha ya kujaribu kuwasiliana naye mara kadhaa bila mafanikio.
Akizungumza kwa masikitiko, mke huyo amesema kuwa Diamond hajibu simu wala meseji wanazomtumia, hata katika kipindi hiki ambacho mume wake, Mkubwa Fella, anaumwa. Amesema hali hiyo imewawavunja moyo, hasa ikizingatiwa kuwa ni Fella mwenyewe anayempigia Diamond lakini hajibiwi kabisa.
Ameeleza kuwa mara ya mwisho Diamond Platnumz kuonyesha msaada kwa familia hiyo ilikuwa mwaka jana walipompeleka Fella nchini India kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa mke huyo, kinachoumiza zaidi ni historia ndefu ya uhusiano kati ya Diamond na Mkubwa Fella, ambapo meneja huyo alisimama naye katika nyakati ngumu za mwanzo wa safari yake ya muziki. Mkubwa Fella anatajwa kuwa miongoni mwa watu waliomshika mkono Diamond, hasa kipindi ambacho baadhi ya vyombo vya habari vilikataa kupiga nyimbo zake.