
Mke wa msanii Bahati, Diana Marua, ameibua gumzo mtandaoni baada ya kujitenga wazi na mwelekeo mpya wa muziki wa mumewe unaohusisha maudhui yanayodaiwa kwenda kinyume na maadili ya jamii.
Kupitia taarifa yake kwa mashabiki, Diana amesema anatambua na anaheshimu safari ya Bahati kama msanii na maamuzi anayochukua kwa ajili ya taaluma yake, lakini akasisitiza kuwa mtazamo wake binafsi ni tofauti. Ameeleza kuwa amejikita zaidi katika biashara, ushirikiano wa kibiashara na chapa zinazomwamini, hivyo lazima aendelee kujiwasilisha kwa njia inayoonyesha uwajibikaji, ukuaji na thamani anazoamini.
Aidha, Diana ameongeza kuwa kwa heshima ya familia yake, washirika wake kibiashara na wale wanaomchukulia kama kielelezo, hatahusika na mwelekeo ambao Bahati amechukua katika muziki wake. Amesisitiza kuwa anaamini katika kupeana sapoti, lakini pia ni muhimu kulinda chapa yake na nafasi ambazo ameendelea kujenga katika tasnia ya burudani.
Diana ametoa kauli hiyo baada ya Bahati kuachia wimbo wake mpya Seti, ujio wake wa kwanza tangu arejee kwenye muziki baada ya mapumziko, ambao hata hivyo umekosolewa vikali kutokana na maudhui yake yanayohamasisha ngono.