LifeStyle

DJ Kezz Awajibu Wanaomkosoa Baada ya Kubadili Dini

DJ Kezz Awajibu Wanaomkosoa Baada ya Kubadili Dini

Aliyekuwa mwimbaji wa muziki wa injili kutoka Kenya, DJ Kezz, amevunja ukimya wake na kujibu vikali wakosoaji wanaomshambulia mitandaoni kufuatia uamuzi wake wa kubadili dini na kuingia Uislamu.

Kupitia mitandao yake ya kijamii, DJ Kezz alitoa ujumbe mfupi lakini mzito, akiwataka wafuasi wake kuheshimu uamuzi wake binafsi. Akiwa thabiti na mwenye msimamo, alisisitiza kuwa ukurasa wake haupaswi kuwa uwanja wa maneno ya chuki au kejeli.

“Ukurasa huu si mahali pa negativity. Kama huwezi kuheshimu safari yangu mpya ya kiroho, basi ni vyema uende zako kimya,” aliandika DJ Kezz kwenye InstaStory yake.

Tangu atangaze kubadili dini, DJ Kezz amekuwa akipokea maoni mseto kutoka kwa mashabiki wake, baadhi wakimpongeza kwa kufuata moyo wake, huku wengine wakionyesha kutoridhishwa. Hata hivyo, msanii huyo ameeleza kuwa imani ni jambo la kibinafsi na hana haja ya kuhalalisha uamuzi wake kwa mtu yeyote.

Hatua ya DJ Kezz kuingia Uislamu imezua mijadala mitandaoni, huku wengi wakitaka kuelewa kinachoendelea katika maisha ya msanii huyo aliyewahi kuvuma kwenye tasnia ya muziki wa injili.

Kwa sasa, DJ Kezz anaonekana kuendeleza maisha yake mapya kwa utulivu, akisisitiza kuwa amani na uhusiano wake na Mungu ndiyo kipaumbele chake kikuu.