
Dj maarufu kutokaTanzania, Romy Jons maarufu Dj RJ, ameibua gumzo baada ya kutoa maoni yake kuhusu malalamiko ya msanii wa Bongo Fleva, Lava Lava. Hii ni baada ya Lava Lava mapema jana kuandika kupitia ukurasa wake wa Instagram kwamba yeye ndiye msanii anayeongoza kwa kufanyiwa fitina kila anapotoa kazi mpya.
Kupitia maoni yake kwenye posti hiyo, Dj RJ alimjibu moja kwa moja kwa kusema kuwa Lava Lava hafanyii fitina bali ukweli ni kwamba nyimbo zake si kali kiasi cha kutikisa sanaa. Aliendelea kumshauri msanii huyo kutafuta mtu wa kumwandikia mashairi, akibainisha kuwa wasanii wengi wakubwa wamekuwa wakifanya hivyo ili kuboresha kazi zao.
Kauli ya Dj RJ imeibua mitazamo tofauti mitandaoni. Wapo waliokubaliana naye wakisema ushauri huo ni wa kweli na unaweza kusaidia Lava Lava kufikia viwango vikubwa zaidi, huku wengine wakimtetea Lava Lava wakidai changamoto anazokumbana nazo ni za kimfumo na zinahusisha chuki binafsi kutoka kwa baadhi ya wasanii wenzake.
Mjadala huu umeendelea kushika kasi, huku mashabiki wakisubiri kuona kama Lava Lava atajibu moja kwa moja ushauri huo au ataendelea kusimamia msimamo wake kuhusu kufanyiwa fitina.