Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Abdulazizi Chende, maarufu kama Dogo Janja, ameapishwa rasmi kuwa Diwani wa Kata ya Ngarenaro katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, hatua inayomuingiza kwenye majukumu mapya ya uongozi wa kijamii.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dogo Janja ameeleza kuwa anamshukuru Mungu kwa kuthibitishwa katika nafasi hiyo pamoja na kupewa majukumu katika Kamati za Mipango Miji, Mazingira na Maadili.
Ameonesha dhamira ya kutumikia wananchi wa Ngarenaro kwa uadilifu, akisema kuwa anataka uongozi wake uongoze kwa maadili mema na kujikita katika maendeleo ya kata na Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa ujumla.
Msanii huyo amesisitiza kuwa uteuzi huo ni heshima kubwa na hatua muhimu katika safari yake ya kujenga jamii kupitia uongozi, huku akiongeza kuwa anahitaji mwongozo wa Mungu ili kutekeleza majukumu yake kwa bidii na uwajibikaji.