Mwanamuziki kutoka nchini Kenya anayevuma na kibao chake “Set It”, Dyana Cods, ameibua mjadala mkali mitandaoni baada ya kuchapisha picha ya skrini inayoonyesha kwamba alimtumia mpenzi wake Ksh 90,000 kama ishara ya upendo.
Kupitia Insta Story yake, Dyana alitoa ujumbe wenye nguvu kwa wanawake, akisisitiza kuwa mapenzi ni ya pande zote, na kwamba wanaume pia wanastahili kutunzwa na kupendwa kwa vitendo.
“Si lazima kila wakati iwe wanaume ndio wanatoa. Wapeni pia. Mkiwapenda, wapeni. Wakijituma, waletee zawadi. Wakinyamaza, shika simu uliza kama wako sawa.”
Ujumbe huu umezua mjadala mkubwa kuhusu nafasi ya wanawake katika mahusiano ya kisasa, hasa katika jamii ambayo mara nyingi huwatarajia wanaume kuwa watoa zawadi na msaada wa kifedha.
Wengi walimsifu kwa kuonyesha mfano wa mapenzi yanayoegemea usawa na kujali kwa pande zote mbili. Hata hivyo, baadhi ya mashabiki walihoji ujumbe wake kwa kuzingatia hali ya maisha ya watu wa kawaida:
“Sisi wengine hatuna hata ya kulipia Wi-Fi, alafu wewe unatuma elfu tisini,” aliandika mtumiaji mmoja wa X (zamani Twitter).
Lakini kuna waliotetea msimamo wake, wakisema ni wakati wanawake waache kusubiri kupokea tu na waanze kuchangia pia pale wanapopenda.
Mbali na kuwa mwanamuziki mwenye kipaji, Dyana Cods amejipatia umaarufu kupitia mitandao ya kijamii kwa mtindo wake wa maisha wa kipekee, misimamo ya moja kwa moja kuhusu mapenzi, na kujiamini kisanaa.
Wimbo wake Set It ulichangia pakubwa kumtambulisha katika muziki wa Kenya, na sasa anaendelea kujijenga kama sauti ya kizazi kipya cha wasanii wanaoelezea maisha yao kwa uhuru – iwe ni kupitia muziki au mitandao.