Msanii nyota kutoka Uganda, Eddy Kenzo, ametangaza mpango wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya promota wa matukio nchini humo Nobart, kufuatia madai mazito ya mauji yaliyotolewa dhidi yake hivi karibuni.
Kenzo, ambaye pia ni mshauri wa rais kuhusu masuala ya muziki, amekanusha vikali madai ya kuhusika na mauji ya msanii chipukizi akiyataja kuwa ya uongo na yenye lengo la kumchafua. Amesema tayari amewasiliana na mawakili wake ili kumshtaki Nobart mahakamani kwa kashfa na uongo wa kuhatarisha heshima yake.
Amesisitiza kwamba promota huyo atalazimika kuthibitisha madai yake mbele ya mahakama kwa kuwa ameyasema hadharani, akiongeza kuwa suala hilo ni zito kwa kuwa linahusu maisha ya watu na sifa ya wasanii nchini Uganda.
Kwa mujibu wa Kenzo, madai hayo yameathiri jina lake binafsi, heshima yake, na uhusiano wake na wadau wa muziki na siasa.
Mwishoni mwa wiki, promota huyo aliibua gumzo kubwa baada ya kudai kwamba rais wa Shirikisho la Wasanii wa Uganda (UNMF), Eddy Kenzo, alihusika katika kifo cha msanii marehemu Danz Kumapeesa, na hata kufikia hatua ya kutaka kumuua yeye binafsi.