
Mwanamuziki na mwanasiasa wa Uganda, Eddy Yaawe, amesema bado hajawa tayari kuingia kwenye ndoa licha ya kuwa na watoto kadhaa kutoka kwa mahusiano tofauti. Akihojiwa na kituo cha televisheni nchini Uganda, Yaawe alieleza kuwa hajawahi kuhofia mahusiano ya kimapenzi, lakini anaamini ndoa ni hatua ya kudumu inayohitaji maandalizi ya kiakili na kihisia.
Yaawe alisema kuwa haoni haja ya kuharakisha ndoa kwa sababu tayari ana watoto, wengi wao wakiwa vyuoni, na maisha yake hayaonyeshi upweke. Alisisitiza kuwa anasubiri kumpata mwenza wa kweli atakayekuwa tayari kushirikiana naye maisha ya kudumu, si kwa shinikizo la jamii au umaarufu.
“Sijawa tayari kwa ndoa; nina watoto, lakini siishi maisha ya upweke. Ndoa si kitu cha kuharakisha. Nataka kuingia kwenye ndoa nikiwa na mtu nitakayeishi naye milele. Nitaoa wakati nikiwa tayari,” alisema Yaawe.
Kauli hiyo imezua maoni mseto kutoka kwa mashabiki na wadau wa burudani, baadhi wakimpongeza kwa uaminifu wake, huku wengine wakitaka aweke mfano kwa vijana kwa kuhalalisha mahusiano. Hata hivyo, Yaawe anaendelea kuwa miongoni mwa wasanii na wanasiasa wenye ushawishi mkubwa nchini Uganda.