Entertainment

Eric Omondi Awataka Wasanii Kusimama na Wananchi Katika Masuala ya Utawala

Eric Omondi Awataka Wasanii Kusimama na Wananchi Katika Masuala ya Utawala

Mchekeshaji na mwanaharakati wa Kenya, Eric Omondi, ametoa wito kwa wasanii kuweka maslahi ya wananchi mbele na kusimama nao katika masuala yanayohusu utawala na mabadiliko ya kijamii.

Kupitia video aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, Omondi amesisitiza kuwa ni wananchi wanaowawezesha wasanii kustawi kwa kuhudhuria matamasha yao na kununua kazi zao, hivyo ni muhimu wasanii nao kuwa upande wa wananchi.

Amesema kuwa kuna upepo wa mabadiliko unaovuma barani Afrika ambao utaifagia mifumo kandamizi, na kwamba yeyote atakayejaribu kuukandamiza ataondolewa. Ameongeza kuwa viongozi na wasanii wanapaswa kumtumikia mwananchi kwani vijana wanapigania mustakabali wao, hivyo wasanii hawapaswi kukaa kimya bali waunge mkono harakati hizo.

Mchekeshaji huyo ameeleza kuwa hali hiyo ni funzo kwa wasanii barani Afrika kuzingatia sauti ya wananchi badala ya kujiweka karibu na mifumo ya kisiasa inayopingwa na raia.

Eric Omondi ametolewa kauli hiyo mara baada ya wananchi nchini Tanzania kupinga kuchaguliwa kwa serikali ya CCM, iliyokuwa ikiungwa mkono na wasanii wengi wakubwa nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *