CEO wa Chama cha Hakimiliki ya Muziki nchini Kenya (MCSK), Dkt. Ezekiel Mutua, ametoa wito kwa wasanii wa Kenya kujikita katika kutengeneza maudhui safi yanayoweza kufurahiwa na familia nzima.
Katika taarifa, Mutua amesema kuwa kazi za sanaa zina nafasi kubwa ya kushirikiana na jamii katika kulea maadili na mshikamano wa kijamii. Ameeleza kwamba wasanii wanapaswa kuzingatia kutoa nyimbo na video ambazo kila mtu, kuanzia watoto hadi watu wazima, anaweza kuzitazama bila wasiwasi.
Dkt. Mutua, anayefahamika kwa misimamo yake thabiti kuhusu maudhui ya sanaa, amesema ataendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha sekta ya muziki inabaki kuwa kioo cha jamii na chanzo cha burudani chenye mafunzo chanya.
Kauli yake inakuja kufuatia kuachiwa kwa wimbo mpya wa msanii Bahati mapema wiki hii, ambao umeibua mjadala mkali mitandaoni kutokana na maudhui yake yenye utata.