
Rapa maarufu wa Marekani, Joseph Cartagena almaarufu Fat Joe, amejikuta kwenye matatizo makubwa ya kisheria baada ya kufunguliwa kesi ya madai inayomuhusisha na tuhuma za unyanyasaji wa kingono dhidi ya wasichana wadogo. Kesi hiyo, iliyofunguliwa tarehe 19 Juni 2025 katika Mahakama ya Wilaya ya Kusini mwa New York, imewasilishwa na Terrance “T.A.” Dixon, aliyewahi kuwa hypeman wake kwa zaidi ya miaka 16.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, Dixon anadai kuwa Fat Joe alihusika katika unyanyasaji wa kingono dhidi ya wasichana wadogo, baadhi wakiwa na umri wa miaka 15 na 16, waliolipiwa upasuaji wa kuongeza makalio (BBL) na kushirikishwa katika matukio ya starehe yaliyohusisha ngono ya kulazimishwa.
Dixon pia anadai kuwa alitumikishwa kwa miaka mingi chini ya hofu ya kupoteza kazi, huku akishuhudia matukio ya unyanyasaji wa kihisia, kifedha, na kimwili. Katika kesi hiyo, anatafuta fidia ya mamilioni ya dola kwa kile anachokiita mateso ya muda mrefu na matumizi mabaya ya madaraka ya Fat Joe katika tasnia ya muziki.
Fat Joe amekanusha vikali madai hayo kupitia wakili wake Joe Tacopina, akisema kuwa kesi hiyo ni njama ya kumchafua na kumlazimisha kulipa fedha kwa njia ya kashfa. Amesema madai hayo hayana msingi wowote na yanaendeshwa kwa nia ya kutafuta umaarufu na pesa kwa njia isiyo halali.
Mbali na kujibu mashitaka hayo, Fat Joe pia ameanzisha kesi nyingine dhidi ya Dixon kwa tuhuma za kuchafua jina lake (defamation), kesi ambayo iliwasilishwa mahakamani mwezi Aprili mwaka huu.
Kwa sasa, kesi hiyo iko katika hatua za awali huku pande zote mbili zikiendelea kuandaa ushahidi na mashahidi wao. Iwapo itabainika kuwa madai yana uzito wa kisheria, Fat Joe anaweza kukabiliwa na matatizo makubwa, ikiwemo hasara ya kifedha, athari kwa jina lake katika tasnia ya burudani, na uwezekano wa mashtaka ya jinai iwapo ushahidi wa moja kwa moja utapatikana.