Sports news

FKF Yasitisha Mechi Zote za Wikiendi Kuheshimu Kifo cha Raila Odinga

FKF Yasitisha Mechi Zote za Wikiendi Kuheshimu Kifo cha Raila Odinga

Shirikisho la Soka Nchini Kenya (FKF) limesimamisha rasmi mechi zote zilizopangwa kuchezwa mwishoni mwa juma hili, kama ishara ya heshima kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Raila Odinga, aliyefariki dunia Jumatano asubuhi alipokuwa akipokea matibabu nchini India.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, FKF imesema kuwa hatua hiyo inalenga kuungana na taifa lote kuomboleza kifo cha kiongozi huyo mashuhuri, ambaye alikuwa mfuasi mkubwa wa michezo na hasa soka. Mechi saba za Ligi Kuu ya FKF (FKF Premier League) zilikuwa zimepangwa kuchezwa wikendi hii kabla ya tangazo hilo kutolewa.

“Shirikisho linaungana na Wakenya wote kuomboleza kifo cha Mhe. Raila Odinga, mwanasiasa mahiri na mlezi wa kweli wa mchezo wa soka nchini,” ilisoma sehemu ya taarifa hiyo.

Kinara wa FKF, Hussein Mohammed, kupitia risala zake za rambirambi, amemtaja marehemu Odinga kama mtu aliyechangia pakubwa kukuza mchezo wa kandanda nchini. Amekumbusha kuwa Raila alikuwa mlezi wa timu ya Gor Mahia, mojawapo ya vilabu kongwe na maarufu zaidi nchini Kenya.

Kifo cha Raila Odinga kimeendelea kuibua hisia kali kote nchini, huku mashirika, taasisi na mashabiki wa michezo wakielezea masikitiko yao kwa kumpoteza kiongozi ambaye aliwahi kuonekana mara kadhaa akihudhuria mechi za soka na kuunga mkono vipaji vya vijana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *