LifeStyle

Gen Z Goliath Afunguka kwa Uchungu Baada ya Kushambuliwa

Gen Z Goliath Afunguka kwa Uchungu Baada ya Kushambuliwa

Kijana aliyejipatia umaaurufu nchini Kenya kupitia kimo chake, Gen Z Goliath, ameibuka na kueleza kwa masikitiko makubwa kuhusu tukio la kushambuliwa kwake pamoja na meneja wake, Francis Juma, wakati wa mechi ya kandanda kati ya FIFA Best FC na Bundes FC katika uwanja wa NCC, Kawangware.

Kupitia ujumbe wa hisia alioweka mitandaoni, Goliath ambaye pia content creator alisema nia yake kuu ilikuwa ni kusaidia kukuza vipaji vya soka mashinani na kuunga mkono vijana kupitia mchezo huo, lakini mambo yaligeuka na kuwa vurugu.

 “Ilikuwa kwa ajili ya upendo kwa soka la mashinani kusaidia mchezo wetu na kuinua wachezaji wa hapa nyumbani. Kwa bahati mbaya, mambo yaligeuka vurugu wakati wa mechi kati ya FIFA Best na Bundes FC. Wahuni walivamia gari langu aina ya Pearl TX na kumshambulia meneja wangu Francis Juma,” alisema.

Kulingana na Goliath, genge hilo la wahuni waliiba KSh 100,000 na vitambulisho vya meneja wake, ingawa kwa bahati nzuri, Juma aliweza kuokoa simu yake. Goliath alisisitiza kuwa soka linapaswa kuwa kiungo cha umoja na si uwanja wa machafuko.

“Soka ni kuhusu umoja, si fujo. Mimi hujitokeza kusaidia kadri niwezavyo, lakini lazima tuelewane hata nyakati ngumu. Tukio hili halipaswi kurudiwa,” aliongeza.

Pia aliwaomba watu wenye moyo wa huruma kusaidia kurudisha kitambulisho cha meneja wake ikiwa watakikuta, akisema ni muhimu kulinda roho ya mchezo wa soka katika jamii.

Tukio hilo limezua masikitiko makubwa mitandaoni, huku wapenzi wa michezo, mashabiki na wanaharakati wa kijamii wakimtaka Goliath kuendelea na juhudi zake japo kwa tahadhari zaidi, huku wakilaani vikali tabia ya vurugu kwenye viwanja vya mashinani.

Polisi bado hawajatoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo, lakini mashinikizo kutoka kwa umma huenda yakachochea hatua kuchukuliwa dhidi ya wahusika.