Mrembo maarufu mtandaoni nchini Kenya, Gloria Ntazola, amefichua kuwa alitumia zaidi ya KSh 1.8 milioni kufanya upasuaji wa kuboresha mwili (cosmetic surgery) mjini Lagos, Nigeria.
Akieleza safari yake ya upasuaji kupitia Instastory, Gloria ametaja kuwa kiasi hicho kilijumuisha gharama za taratibu za kitabibu, malazi ya hoteli, huduma za uangalizi baada ya upasuaji, pamoja na matibabu ya ziada aliyohitaji wakati wa kurejea katika hali yake ya kawaida.
Hata hivyo, licha ya kushiriki uzoefu wake, mrembo huyo anayejulikana kama Kanjo Lady, ametoa tahadhari kwa wafuasi wake kuhusu hatari zinazohusiana na upasuaji wa aina hiyo.
Gloria amesisitiza kuwa upasuaji wa kubadilisha mwonekano si jambo la mzaha na unaweza kuhatarisha maisha, akiwataka wanaofikiria kupitia njia hiyo kujiandaa kisaikolojia, kifedha na kimwili kabla ya kufanya uamuzi wowote.